Tarehe 24.09.1992 ni siku ambayo hawezi kuisahau katika maisha yake. Ni siku ambayo alimpoteza Baba yake mzazi ambaye ndiye alikuwa tegemeo la familia katika nyanja zote za maisha.
Katika siku za mwisho za uhai wa baba yake alipewa usia kwamba aitunze familia yake; hivyo kwenye wimbo wa “Hayakuwa Mapenzi” aliposema “Baba alipofariki ilibidi nimtunze mama na zaidi kuhakikisha wadogo zangu wanasoma” haikuwa mistari tu alikuwa anazungumzia maisha yake halisi.
Usia aliohusiwa na baba yake ulimpelekea mwaka 1993 kuzamia nchini Afrika Kusini lakini kutokana na nchi hiyo kujiandaa na uchaguzi mkuu mwaka 1994 idara za usalama zikaamua kufunga mipaka yote ya nchi,hivyo juhudi zake za kuingia Afrika Kusini zikagonga mwamba na kuamua kurudi nyumbani na baada ya muda kidogo akapata kazi ktk kituo cha mafuta cha BP kilichopo Kurasini.
IkumbukweTangu akiwa shuleni, alikuwa akijihusisha na muziki, hivyo alipopata ajira BP akaingia studio kwa mara ya kwanza na kurekodi Wimbo wa Siku Yangu, akitumia jina la 2 Proud na baadaye kukamilisha albamu yake ya kwanza iitwayo Ni Mimi iliyomtambulisha vyema kwenye muziki.
Baadaye alisimamishwa kazi BP, akazamia Ulaya nchini Uingereza kwenye mji mdogo wa Slough, nje kidogo ya London alikopata kibarua kwenye kiwanda cha kutengeneza dawa za meno. Alikaa kwa miaka kadhaa kabla ya kurejea Bongo kuendelea na harakati za muziki.
Inawezekana akawa ndiye msanii wa kizazi kipya mwenye album nyingi. Mpaka sasa ametoa album takribani tisa. Album hizi ni kama “Ni Mimi” iliyotoka mwaka 1995, Ndani ya Bongo (1996), Niite Mr II (1998), Nje ya Bongo (1999), Millennium (2000), Muziki na Maisha (2001), Itikadi (2002), Sugu (2004), Coming of Age-Ujio Wa Umri (2006) na VETO iliyotoka mwaka 2009.
Mwaka 2010 aliingia rasmi kwenye siasa baada ya kuchukua kadi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kugombea ubunge wa Jimbo la Mbeya Mjini, akashinda na kufanikiwa kuingia bungeni. Mpaka sasa ni Mbunge wa Mbeya Mjini ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo.
Huyo ni Joseph Mbilinyi a.k.a Mr Two a.k.a Sugu ameandika historia ya maisha yake kwenye kitabu kiitwacho “ MUZIKI NA MAISHA”- FROM THE STREET TO PARLIAMENT.
Kitabu Chake |