Teknomovies Inspirational : Somo la Bill Gates kwenye mafanikio - teknomovies
Teknomovies Inspirational : Somo la Bill Gates kwenye mafanikio

Teknomovies Inspirational : Somo la Bill Gates kwenye mafanikio

Share This

Bill Gates ni mwekezaji wa Marekani, Programa wa Kompyuta na mwenyekiti wa zamani wa kampuni ya Microsoft (Kampuni kubwa ya programu duniani). Tangu mwaka 1995 amekuwa tajiri namba moja duniani kwa mujibu wa jarida la Forbes isipokuwa mwaka 2008 ambapo alikuwa namba 3. Unaweza usijue lakini kila sekunde Bill Gates anaingiza takribani dola 250 za kimarekani na kwa dakika nzima anaingiza takribani dola 15,000. Unashangaa? huyo ndio Bill Gates. Sasa tujifunze somo la mafanikio kutoka kwa Tajiri huyu.



1. Bill Gates alianza kujishughulisha na maswala ya kompyuta alipokuwa na umri wa miaka 13. 

Hili linatupa somo muhimu la kuanza mambo mapema. Unapoanza jambo mapema unajijengea uwezo zaidi wa kukomaa kwenye jambo husika pia kwa kuanza jambo muda mrefu unajijengea uzoefu ambao utakukinga dhidi ya kukata tamaa.

2. Hutakuwa tajiri mara baada ya kumaliza shule.

Bill Gates alifahamu kuwa hawezi kupata pesa kwa kiwango kizuri mara baada ya kuhitimu elimu yake ndio maana akaamua kuacha chuo. Siku hizi haijalishi una cheti kizuri kiasi gani, hutoajiriwa kuwa Mkurugenzi wa kampuni ya kimataifa au kazi nyingine kubwa kabla ya kujenga uzoefu. Hili ni somo zuri ambalo kila mhitimu au msomi anaweza kulitafakari ili limsaidie katika kufanya maamuzi.

3. Fanyia kazi ndoto zako 

Mfanyabiashara na Mwandishi wa vitabu Farrah Gray aliwahi kusema "Jenga ndoto zako wewe mwenyewe, la sivyo mtu mwingine atakuajiri kujenga zake". Bill Gates alianza kufanyia ndoto zake mwenyewemapema bila kujali changamoto wala vikwazo.

4. Kujifunza kutokana na makosa

Ukiharibu sio kosa la wazazi wako kwa hiyo usilie kutokana na makosa yako bali jifunze kutokana na makosa hayo. Bill Gates anasema kuwa makosa ni shule nzuri sana inayotuwezesha kuboresha maisha na ufanisi wa kile tunachokifanya. Gates anatukumbusha umuhimu wa kujifunza kutokana na makosa hayo ili wakati mwingine yasitokee.

5. Kujitoa na kuwa na Subira

Ni wazi kuwa mafanikio ya Bill Gates hayakuwa ya usiku mmoja wala rahisi kuyapata. Ni ukweli usiopingika kuwa alifanya kazi kwa bidii kwa miaka mingi bila kukata tamaa wala kukosa uvumilivu. Tunakosa vitu vingi kwenye maisha yetu kutokana na kutokujitoa pamoja na kukosa uvumilivu katika yale tunayoyafanya.

6. Televisheni sio maisha halisi 

Mara nyingi tumekuwa tukiona watu wakiishi maisha ya kifahari au anasa mbele ya kamera. Lakini uhalisia wa maisha hauko hivyo, maisha yana changamoto na inatupasa kuzikabili. Televisheni sio maisha halisi watu wanatakiwa kuacha kuigiza na badala yake kufanya kazi.

7. Maisha hayana usawa

Haijalishi unafanya kazi gani na kwa bidii kiasi gani , wakati mwingine mambo yanaweza yasiende kama unavyotarajia. Bill Gates anatukumbusha kuwa hakuna watu wakioandikwa kufanikiwa au kupata kitu fulani, hivyo wakati mwingine tukubaliane na hali halisi.

8. Kuwa tayari kukabili hatari.

Kuanzisha biashara ni jambo lenye changamoto au hatari nyingi. Unaweza kuwa na pesa nyingi pamoja na wazo zuri la biashara lakini ukaishia kupata hasara. Bill Gates anatukumbusha kuwa biashara ni kuthubutu, kuchukua au kukabili hatari au changamoto. Gates anasema Biashara ni mchezo wa pesa wenye kanuni chache na hatari nyingi.

9. Hakuna njia ya mkato ya mafanikio.

Watu wengi hujidanganya kuwa kuna njia ya mkato ya mafanikio au kufanikiwa au kupata pesa. Katika uhalisia hakuna kitu cha namna hiyo. Bill alianza Microsoft miaka mingi iliyopita pamoja na rafiki yake Paul Allen hadi leo hii ambapo ni tajiri namba moja duniani. Gates anasema uvumilivu ni kipengele muhimu cha mafanikio.

10. Jikubali ulivyo.

Watu wengi wanakosa furaha pamoja na kushindwa kufikia malengo yao kutokana na kutojikubali wao wenyewe. Bill Gates anatukumbusha kutokujilinganisha na watu wengine, kwani kwa kufanya hivyo tunajfanya kuwa duni sisi wenyewe. Gates anasema usijifananishe na mtu yeyote katika ulimwengu huu, ikiwa unafanya hivyo unajidunisha wewe mwenyewe.

Kwa hakika kuna mengi ya kujifunza kutoka kwa watu waliofanikiwa ikiwa tunataka kufanikiwa kazi iliyobaki ni kuweka kwenye matendo.

Uwe na wiki njema yenye mafanikio.

No comments:

Post a Comment

Pages