"Sipendi Siasa Sababu Inatengeneza Marafiki Wanafiki," Wakazi - teknomovies
"Sipendi Siasa Sababu Inatengeneza Marafiki Wanafiki," Wakazi

"Sipendi Siasa Sababu Inatengeneza Marafiki Wanafiki," Wakazi

Share This
Rais wa Marekani Donald trump anaonekana kuwa ni kati ya Rais ambao ni wakorofi na wasiopenda kuingiliwa katika mambo yao, lakini msanii Webiro Noel Wasira ‘Wakazi’ yeye alikuwa miongoni mwa watu waliowahi kukutana na Rais huyo wa sasa nchini Marekani.

Wakazi ni msanii wa miondoko ya Hip Hop ambaye alikuwa akiishi nchini Marekani kwa muda mrefu, na kupata uzoefu wa nchi mbili tofauti kuanzia katika maisha ya muziki mpaka maisha ya kawaida nje ya Muziki.

Mwananchi ilifanya naye mazungumzo kutaka kufahamu mengi juu yake kutokana na kuwa ni miongoni mwa wasanii ambao waliweza kupafomu katika jumba la Big Brother sehemu ambayo ni ngumu msanii wa kawaida kuipata.

ILIKUAJE KUTUA MAREKANI

“Nilienda kusoma Marekani lakini nilivyoenda kule nikajikuta naendelea na Muziki kitu ambacho nilikuwa nakipenda tangu nikiwa nakaa Tanzania, na watu wakubwa waliokuwa wakinifanya nipende Muziki ni watu mtaani kwetu takishari kwasababu kwa miaka ya nyuma mtaa huu walikuwa wanakaa mabalozi,”anasema.


“Hivyo nilivyoenda kusoma ikawa nafanya kitu ambacho nakipenda kila siku lakini nashukuru Mungu nilikuwa nakifanya kwa umakini mkubwa, nilihakikisha kuwa najulikana kule na hata nyumbani kwasababu unatakiwa uwe unajulikana kuanzia nyumbani,”anasema.

ALIKUTANA VIPI NA TRUMP

“Nilivyokaa kwa miaka kadhaa maisha yalibadilika na ukiangalia kuwa upo katika nchi ya watu, hivyo ikanibidi nianze kufanya kazi katika jengo la Trump ‘Trump Tower’ na ndipo ambapo nilikutana na Trump na sio yeye pekee, kwani jengo lile lilikuwa likitembelewa na watu wengi mno maarufu hivyo nikawa nakutana na wasanii wakubwa pia,”anasema.

“Trump kwa kipindi chote ambacho nilikuwa nikifanya kazi ndani ya jengo lake, nimeona ni mtu ambaye anajali watu na ni msikivu ila ukifanya kitu ambacho hajakipenda ni mtu ambaye anachukua maamuzi ya haraka mno,”anasema.

ALIWEZAJE KUJIPANGA KATIKA MASOMO,MUZIKI NA KAZI

“Ilikuwa ni wakati mgumu sana kwangu kwa namna moja ama nyingine, kwasababu nilikuwa nchi ya watu na nilitakiwa niishi vizuri hivyo licha ya kuwa nilikuwa ni mwanafunzi kule lakini ilibidi nijichanganye,”anasema.

“Nilikuwa najipanga kuwa asubuhi kama nitaenda chuo basi nikirudi napumzika, alafu naingia kazini katika upande wa muziki ilikuwa sio shida sana, lakini inapotokea ishu ya kusafiri kwenda kufanya shoo ndio ilikuwa changamoto kwasababu ilikuwa unatoka mji mmoja kwenda mji mwingine,kuna kipindi niliacha mpaka Chuo”.

TOFAUTI YA HIP HOP YA BONGO NA MAREKANI

“Mziki haunaga tofauti yoyote, bali ni kuwa hapa nyumbani haijatengenezwa fomula nzuri, kupigwa Muziki redioni haimaanishi kuwa umeuza, Kuna watu wanakuwa na mixtape nyingi kule Marekani na wanapiga pesa kuliko ambao wana nyimbo zao redioni, kitu ambacho ni tofauti na hapa nyumbani,”anasema.


Pia aliongeza kuwa wasanii wengi wanakuwa na Identity (Utambulisho) yao ya kutambulisha sehemu wanayotokea kama ambavyo alikuwa anafanya 50 Cent, Fat Joe kwa kutaja sehemu ambayo wanatokea na kisha watu wanaokaa maeneo hayo kuanza kuwasapoti kwa kununua mixtapes (Kanda Mseto) zao.

ALIPATAJE NAFASI YA KUPIGA SHOW BBA

“Ile nafasi wengi hawakutarajia kama ningeipata, kutokana na kuwa nyimbo zangu hazipigwi sana katika redio za nyumbani, lakini nilichokuwa nakifanya mimi kwa miaka ile ni kuhakikisha kuwa naweka kazi mitandaoni , ukitafuta msanii ambaye anatoka Tanzania nilikuwa nipo katika orodha hiyo na wakati ule Big brother walikuwa wanataka msanii ambaye anachipukia kutoka Tanzania hivyo walivyotafuta waliniona mimi,”anasema.

ANAAMINI MITANDAO INALIPA

“Mitandao inalipa ndio kwasababu kama mtu akisikiliza wimbo wako kupitia akaunti yako wewe pesa inaongezeka, utaitwa na kwenda kusaini na kisha kuchukua pesa yako, na hicho ndicho kitu ambacho mimi nakifanya,”anasema.


Pia aliongeza kuwa kupitia mitandao inakuwa ni rahisi kufanya wimbo na msanii kutoka nje kutokana na kufatilia kazi zako katika mtandao na kisha kukutafuta, ni tofauti na kupigwa katika redio za nyumbani huku wasanii wa nje hawasikii kazi zako.

BIFU LAKE NA GODZILA LIMEKAAJE

“Mimi na Zilla hatuna bifu la nje ya maisha ya kawaida, lakini kilichotokea ni kuwa mimi nilitweet kwenye Twitter na yeye akaja kukomenti kitu asichokijua na mimi nikamjibu hivyo watu wakaona yale mazungumzo yetu ghafla yakawa makubwa mno”anasema.

“Nikapelekwa katika kituo kimoja cha Redio kwenda kumaliza ubishi nay eye kwa kufanya mitindo huru na nilifanikiwa kufanya vizuri dhidi yake, na baada ya hapo ikanibidi nitoe wimbo kuhusu yeye na yeye akatoa wimbo kuhusu mimi yani ndio ikawa hivyo,”anaelezea.

NGUVU YA UMENEJA WA LADY JAYDEE

“Wengi hawajui kuwa mimi na Jide ni mtu na binamu yake, hivyo kuwa meneja ilitokea tu baada ya kuwa aliyekuwa meneja wake kuacha kazi hiyo na kutokana na ukaribu wangu na kujua ufanyaji wetu wa kazi ikabidi anikabidhi jukumu hilo, lakini nashukuru nimelifanyia kazi vizuri eneo hilo,”anasema.

“Katika kipindi chote ambacho nimefanya kazi nimejifunza vitu vingi, hakuwahi kunisumbua kwasababu ni mtu ambaye anajielewa sio msanii mpya, na kuwa naye karibu kumenikutanisha na watu wengi na hata mimi pia nilikuwa natumia nafasi hiyo kutangaza kazi zangu,”anasema.

KWANINI SHOO ZA HIP HOP ZINAKUWA NA VIINGILIO VIDOGO

“Uzuri ni kwamba nimeshakuwa meneja wa Jaydee kwahiyo najua kabisa kuwa upande wa pili wa shilingi wanafaulu vipi, kikubwa ukiwa unataka kuweka kiingilio kikubwa unatakiwa uonyeshe jinsi ambavyo ela yao inavyotumika”, anasema.


Aliongeza kuwa huwezi kuweka kiingilio kikubwa na ukawa hauna vitu vingi kama live band, hivyo ni muhimu kuhakikisha kuwa unakuwa na vitu vingi ambavyo hata mtu anayetoa pesa yake anapata kitu kinachoendana, ila kwa upande wetu sisi kiukweli bado inabidi nguvu iongezeke zaidi japokuwa katika matamasha makubwa,huwa tunafanya vitu vikubwa hasa kwa kutumia sauti halisi bila Cd.

AWAKATAA KIAINA MADIREKTA WAKUBWA

“Naweza kusema kuwa nilikuwa na mtayarishaji mkubwa Hefemi ambaye ni Mtanzania anayeishi Marekani, yeye ndio alikuwa anatayarisha kazi zangu nyingi nilipokuwa nje ya nchi lakini hata niliporudi alikuwa anatayarisha na kazi zilikuwa zinafanya vizuri,”

“Uzuri wa kazi sio mtayarishaji mkubwa kwani baada ya Hefemi nilihamia kwa Meck Kaloka ambaye nilimsihi aongozane na Hefemi ili ajue aina ya video zinazohitajika na ndio maana mpaka hivi sasa video zangu zinafanya vizuri, na kupitia Meck  Kaloka nyimbo ya ‘Dengue Fever’ ambayo niliifanya kwa gharama ya chini lakini ilinifanya niingie katika tuzo za Kora,Tuzo ambazo ni kubwa mno kwa hapa Africa,”anasema.

ANAMZUNGUMZIAJE HASHEEM THABEET

“Alikuwa ni mtu mzuri kwangu kwasababu tulikuwa tunaishi vizuri tulipokuwa wote Marekani, na ilifika kipindi hata natakiwa niende katika mji mwingine alikuwa akinisaidia hata mafuta ya kunisogeza, na hali hiyo iliendelea mpaka alipoingia NBA ni mtu mzuri sana na niliishi  nae vizuri,”


“Najua kuwa hivi sasa anajifua na mazoezi binafsi ili aweze kurudi katika NBA, ila ni ngumu sana na yeye analijua na Watanzania wanaoishi kule wanalijua kwasababu kupata nafasi NBA ni mpaka mtu aumie au kiwango chake kishuke, hivyo ataangalia kama hatopata pale nafasi anaweza akatafuta sehemu nyingine,”anasema.

UPANDE WA SIASA YUPOJE

Wakazi licha ya kuwa anamuita Baba Mdogo Steven Wasira, yeye amefunguka kuwa hajihusishi na Siasa kutokana na siasa kuwa na mambo mengi, pia siasa inakuwa aina marafiki wa kweli ambao wanaweza kumsaidia mtu katika kipindi anachohitaji.

“Mimi Siasa ya Jamii, Uraia sijihusishi nayo kabisa, najihusisha na siasa ya nchi kwasababu mimi ni mfanyabiashara na biashara yangu ni muziki, na mziki ninaofanya ni siasa pia kwasababu ni mziki wa kweli na upo wazi, katika upande wa kupiga kura huwa naangalia utendaji wake wa kazi na ndio napiga kula lakini huwa siangalii chama,”

WASANII ANAOWAKUBALI KUPITIA IDADI ZAO ZA KAZI

Wakazi alisema kuwa wasanii anaowakubali ni watano na ni kutokana na idadi zao za kazi ambazo wamezifanya mpaka hivi sasa, huku wakiwa wanaendelea na muziki kama kawaida hivyo ni ngumu kufikiwa.

“Wasanii Prof J,Sugu,Fid Q,Mwana Fa,Nikki Mbishi ni kati ya wasanii ambao wanazingatia sanaa na vigezo, lakini pia ni wasanii ambao wana idadi kubwa ya kazi zao nikimaanisha albam tangu waanze Muziki ndio wanaongoza kwa kuwa na albamu nyingi,”anasema.

MWISHO


No comments:

Post a Comment

Pages