IJUE HALLOWEEN NI NINI NA IMETOKA WAPI - teknomovies
IJUE HALLOWEEN NI NINI NA IMETOKA WAPI

IJUE HALLOWEEN NI NINI NA IMETOKA WAPI

Share This
Kwanza niwatakie heri ya mwezi mpya wa Novemba Tumebakiza miezi miwili tu tumalize mwaka 2017 ila vyuma vimekaza kinoma muhimu ni kumomba Mungu tumalize mwaka salama na tutimize malengo yetu....Ameen ...!!!!



NOVEMBA 1 kila mwaka ni siku maalum kwa ulimwengu wa Magharibi kuadhimisha Siku ya Maruhani ambayo kwa Kiingereza inajulikana kama ‘Halloween’.


Unapoitafuta maana halisi ya sherehe hii utakutana na maana nyingi zikiwa na mrengo tofauti tofauti. Kubwa ni kuwa chimbuko la Halloween ni sherehe ya kipagani iliyokuwa ikifanywa na watu waitwao wacelts miaka 2000 iliyopita. 

Wacelts kwa miaka ya leo wanatajwa kuwa ni watu wa Ireland, Scotland, Brittany, Wales na kadhalika kwa kuwa chimbuko la lugha ya celts iko ndani ya mataifa haya. Wacelts walikuwa na sherehe inayoitwa Samhain inatamkwa ‘Sawin’. Sherehe iliyokuwa inahitimisha kipindi cha mavuno na kuanza kwa majira ya baridi, kuanza kwa mwaka mpya. Kipindi hicho cha baridi kilikuwa kinaitwa ‘Darker Half of the year’ yaani kipindi cha mwaka kisicho na nuru kulingana na kalenda ya wacelts, walipoanza majira hayo walikuwa wanaanza mwaka mpya kwao.
Wacelts
Wacelts walikuwa wanaamini kwamba wafu wanaweza kutembea katikati ya watu walio hai. Na wakati huu walipokuwa wanamalizia mavuno na kujiandaa na majira ya baridi ya mwaka mpya, wacelts waliamini usiku huo kabla ya mwaka mpya mpaka unaowatenganisha walio hai na wafu huwa unatoweka hivyo mizimu ya wafu huja duniani tena. Na wanaporejea husababisha majanga mengi ikiwemo kuharibu mavuno yao. 

Lakini pia waliamini mizimu hii inapokuja duniani tena huwasaidia watabiri kutabiri mambo yao katika mwaka huo wa baridi na giza. Waliamini kwenye kutoa kafara na kuacha vyakula nje ya nyumba zao au kutoa vyakula na wanyama kwa ajili ya kafara. Mizimu yenye roho nzuri itawasaidia kukivuka kipindi cha baridi salama. Pia wacelts walitembelea makaburi ya ndugu zao, wakafanya ibada na matambiko yao wakiamini wafu wangeweza kuwatabiria yajayo. 

Kwa kipindi hicho watababiri walikuwa watu muhimu mno na walioaminiwa na kutumainiwa kutoa mwongozo wa mambo yajayo. Katika kuadhimisha hii siku, watabiri hao walitengeneza moto mkubwa. Wenzetu wanaita Bonfire. Ambapo watu walijumuika kuchoma mazao na wanyama kama matambiko kwa miungu ya Wacelts. Walipokuwa wakifanya hivi, walivaa mavazi rasmi ya kutambikia miungu… vichwa vya wanyama, ngozi za wanyama. Wengine walivaa mavazi ya kutisha ili kuwachanganya mizimu wadhani na wao ni mizimu wenzao hivyo wasiwadhuru kwa namna yoyote ile wanapokuwa nje usiku wa samhain. Wengine waliwapa mizimu pipi na vitu vitamu ili kuwatuliza isiwadhuru.

Bonfire
Mwaka 43 A.D Ngome ya Rumi ilifanikiwa kuiweka Celtic chini ya utawala wake kwa miaka 400 (mia nne) dadeeeki!.... hivyo sherehe mbili zenye asili ya rumi ziliunganishwa na sherehe ya Samhain ya waceltic. Sherehe ya kwanza iliyoitwa Feralia ambayo ilisherehekewa na warumi siku za mwisho za mwezi Oktoba ambapo warumi waliadhimisha siku ya kukumbuka waliotangulia (wafu). 
Na sherehe ya pili ilikuwa ni sherehe ya heshima ya muungu wa matunda na miti aitwaye Pomona. Alama ya Pomona ni Apple na sasa ukijumlisha hizi sherehe mbili na Samhain ya waceltic unapata kwanini Kwenye Halloween kuna mchezo wa Bobbing apple!... huu mchezo huchezwa wakati wa Halloween hususani na watoto ambapo maji hujazwa kwenye beseni au bakuli…. Apples hutumbukizwa kwenye maji na yanapoelea kwenye maji. Unatakiwa uokote apple kwa mdomo na sio kwa mikono. Tena wengine mikono hufungwa nyuma kabisa ili usifanye udanganyifu. 
Mchezo wa Bobbing Apple

Umeanza kuelewa kuhusu Halloween eeeh!! May 13 609 A.D Papa Boniface IV aliligeuza jumba la miungu ya kirumi kuwa la kikatoliki kwa heshima ya mashahidi wa imani ya kikatoliki. Inasemekana hili ndilo jumba la kwanza la kipagani kubadilishwa kuwa Kanisa la kikristo. Aliyeunda mchoro wa jengo hili anaitwa Marcus Agrippa aliliunda kwa heshima ya miungu wote wa kirumi.



Rome Pantheon mpaka sasa bado ipo
Sikukuu ya wakatoliki ya All Martyrs day ilikuja kuanzishwa rasmi na Papa Gregory III (731-741) na baadaye ikahusisha pia watakatifu pamoja na mashahidi/ mashujaa wa imani na ikaondolewa toka May 13 na kuwa Nov 1. Kufikia karne ya 19, ukristo ulishaenea zaidi kwenye jamii ya waceltic na kufanya waceltic waunganishe baadhi ya mila zao na mila ngeni kwao za ukristo. 

Inasemekana Kanisa lilikuwa linajaribu kuiua Samhain ya kipagani kwa kufanya maadhimisho yenye mrengo wa kitakatifu kwa mfano Souls day (sijui nitafsirije)…ilisherehekewa kimfanano na Samhain. Watu walivaa kama watakatifu, malaika wakawasha bonfire pia. Na Siku ya watakatifu ilikuwa inaitwa all hallows au all hallowsmas ikiwa na maana All Saints!!...sasa ule utamaduni wa usiku wa Samhain katika eneo la waceltic nao ukaanza kuitwa All-hallow Eve na hatimaye likaja neno Halloween!!... utamaduni wa Samhain uligoma kuisha pamoja na Ukristo kuingia katika jamii ya Waceltic. 

Walijitahidi kuukubali ukristo hapa na pale lakini walishindwa kuacha imani zao za kipagani na hivyo wakaamua kuzichanganya changanya na ukristo kukidhi mahitaji yao!! Na ndio Samhain yao ilivyogeuka Halloween!! Umepata jibu kwanini Halloween inahusishwa na ukristo??.... ni vile tu watu hatuelewi historia ya Halloween! Hivyo wapagani walioletewa ukristo walilichukua neno all hallows lenye maana ya watakatifu…neno ambalo lilitumika siku ya watakatifu ya wakatoliki …. wakaliweka katika sikukuu yao ya kipagani na hatimaye wakapata jina lao la Halloween!!.


Wahamiaji toka maeneo ya Waceltic walipohamia bara la Amerika, waliingiza utamaduni wa Halloween pia. Ndio hivi leo hata wamarekani wanaadhimisha Halloween. Ilipoingia Amerika, Halloween ilibadilika taratibu. Safari hii maadhimisho yaliongezewa manjonjo kama michezo, na sherehe ya mavuno ambapo majirani walikutana na kushea hadithi za wafu na hadithi za kutisha. 

Wakitembelea watabiri kusikiliza maajaliwa yao, waliburudika kwa kuimba na kucheza. Kipindi cha karne ya 19, Amerika ilipata wahamiaji wengi zaidi. Wahamiaji hawa ambao wengi walitoka Ireland ambao walikuwa wanakimbia janga la ukame mwaka 1846, walisaidia kuongeza umaarufu wa Halloween kwa kuwa ni watu waliotoka katika jamii ya waceltic. Waamerika nao wakaanza kuvaa mavazi ya Halloween wakipita nyumba hadi nyumba kuomba chakula na pesa kama sehemu ya kusherehekea Halloween. 

Kumbuka utaratibu huu ulitoka kwa waceltic ambao walipita nyumba hadi nyumba wakiomba mazao na wanyama ili wakatoe kafara zao kipindi kileee mwanzo. Utaratibu huu ndio ukaja kuwa Trick and treat ya leo inayofanyika Halloween. Trick and treat ni kwamba watoto wanapita nyumba hadi nyumba wakikusanya pipi, biskuti wengine wanatoa pesa. Trick ni kitisho tu kuwa usipotoa watakufanyia mazingaombwe. Treat ndiyo hiyo unawapa ili wasikufanyie mazingaombwe.
 
Watoto wakipita kukusanya Pipi

 Miaka ya 1800 mwishoni, Halloween ilianza kubadilika zaidi. Ikajumuisha jamii kwa ujumla ambapo ikawa kama get together party…yaani party ya pamoja zaidi kuliko mambo ya kusimuliana mambo ya wafu na mizimu au uchawi. Michezo mingine ikabuniwa. Vyakula vikaletwa pamoja, na vyombo vya habari vikaomba wazazi wapunguze mavazi ya kutisha au michezo ya kutisha sana ili kutoshtua watoto. 

Maono kama haya yakachangia sana kuifanya Halloween ipoteze ile sifa kubwa ya kuihusisha na uchawi na wafu. Miaka ya 1920 – 1950 Halloween ilianza kuingia hadi mashuleni. Siku ya Halloween watoto walivaa mavazi ya ajabu ajabu, wengine wakiigiza watu maarufu, wengine wakivaa kama wanyama na kadhalika Na ndio wakati huo trick and treat ile ndio ikapamba moto. Na hapa sasa Halloween ikawa utamaduni mpya wa waamerika mpaka leo hii!! Leo hii Waamerika ndio wanaongoza kwa kusherehekea Halloween. 

Wakiipamba kwa matangazo na mbwembwe zingine nyingi za kibiashara zaidi kuliko imani maana mavazi ya Halloween yanakuwa ya kuiga watu maarufu badala ya mizimu...wengine huvaa character za wahusika katika filamu kama spiderman au Batman.


Naimani umefahamu japo kwa uchache kuhusu Halloween na kwa nini inasherehekewa sana katika nchi za magharibi hususan Marekani. Basi bhana nikutakie Halloween njema.

Source : Wikipedia na mitandao mbalimbali 

Usisahau Kutufollow Instagram na Twitter @Teknomovies kwa Updates mbalimbali lakini pia Subscribe Youtube channel ya DM Online Tv.










Jengo la Rome Pantheon ambalo mpaka leo lipo kabisaaa Na mbele lina chapa ya Marcus Agrippa iliyowekwa na Hadrian aliyelimalizia Mwaka 125 CE wakati wa utawala wake.

Cheap Offers: http://bit.ly/gadgets_cheap
















Kwanza niwatakie heri ya mwezi mpya wa Novemba!

Cheap Offers: http://bit.ly/gadgets_cheap

Pages