Aslay:Nina Nyimbo Nyingi Zaidi Hata Ya Watu Wanavyofikiria#Mahojiano - teknomovies
Aslay:Nina Nyimbo Nyingi Zaidi Hata Ya Watu Wanavyofikiria#Mahojiano

Aslay:Nina Nyimbo Nyingi Zaidi Hata Ya Watu Wanavyofikiria#Mahojiano

Share This
Ilinichukua masaa matano kuweza kukutana na Aslay,huku masaa manne yakipotea kwa kumsubiri na moja likitumika kwa kazi maalumu ambayo ndiyo ilinifanya nimtafute na kumsubiri, na si kingine bali ni mahojiano.
Kwa sasa jina la Aslay kwa Bongo,lipo katika levo za juu na hii inawezekana ikawa ndiyo sababu ambayo kuweza kupata nafasi ya kufanya nae mahojiano yakupasa uwe mvumilivu sana sababu ya ubize mkali kutokana na kuzunguka mikoa mbalimbali kupiga shoo huku akifanya mambo mengine mbalimbali ambayo hapendi kuyaweka wazi.

“Aisee pole sana ndugu yangu kwa kukuweka sana,” Alianza Aslay mara baada ya kuonana nae huku nae akionekana kuchoka ambapo alianza kwa kulalamika njaa .

Mahojiano yalianza mara moja sababu kwa saa lingine ambalo lilikuwa linafuata alikuwa anatakiwa eneo lingine hivyo haikutakiwa kulaza damu.

Kwanini Nyimbo Mfululizo?

Moja ya kitu ambacho wengi wamekuwa wakitaka kujua ni kwanini anaachia ngoma mfululizo,ambapo mpaka sasa ameachia video saba huku kila video ikipishana kwa mwezi mmoja mmoja,kwa maana kwamba kila baada ya mwezi kupita amekuwa akiachia video.Video hizo ni kama Angekuona,Baby,Usiitie Doa aliyofanya na Khadija Kopa,Muhudumu,Pusha,Likizona Natamba Na kwa upande wa Audio mpaka sasa kupitia akaunti yake ya Youtube zipo kumi na mbili tu ambazo ni Pusha,Usiitie Doa,Baby,Danga,Koko,Rudi,Hutegeki,Muhudumu,Likizo,Marioo,Natamba na Tete,lakini zinazidi idadi hiyo kwa sababu kuna nyimbo nyingine ambazo zipo mitaani kama Nyakunyaku pamoja na singo kadhaa.

Akijibu hilo Aslay anasema kwake anafanya hivyo kwa sababu anaamini muziki mzuri hauwezi kufa hata kidogo.

“Kwanza Muziki mzuri haufi hata siku moja lazima watu wajue,na kingine mimi nimeamua kuachia nyimbo mfululizo sababu nilitaka kuwa na nyimbo za kutosha hata nikienda kufanya shoo mashabiki zangu waweze kufurahi nyimbo zangu na sio tena za Ya Moto Bendi,”
“Na pia nilipoteza flash yenye nyimbo lakini ilikuwa muda sana japo niliogopa kwamba nyimbo zangu zisije kuanza kuvuja lakini namshukuru Mungu haikuwa hivyo ila sababu kubwa ndio hiyo niliyosema,”
“Na kuhusu kuendelea ama kuacha kuachia ngoma kama hivi hiyo ndio fomula yangu ila nitakuwa naangalia upepo unaendaje sababu wasinione mjinga pia,”

Meneja wake kwa sasa?

Baada ya kuachana na Mkubwa Fella,Aslay anasema kwa sasa kazi zake anasimamiwa na Chambuso hivyo kwa watu ambao walikuwa wakifikiri kwamba hana msimamizi yeyote ndio waanze kujua hilo.
“Huyu ndio meneja wangu kila kitu kuhusu muziki wangu na mambo mengine mbalimbali yeye ndiye anasimamia, nashukuru anafanya kile ambacho nakipenda haswa,”

Kuhusu Nyumba?

Katika suala la Nyumba ambazo inadaiwa walikuwa wakijengewa kipindi wapo Yamoto na kuna tetesi zilikuwa zikiendelea kuwa Nyumba hizo ziliota mbawa,Aslay anajibu kuwa nyumba hizo zipo na si kweli kama wengi walivyokuwa wanasema.

“Nyumba zipo tulijengewa wote Mbagala eneo moja na mpaka sasa naweza kusema zina hadhi kweli ya mtu kuishi,”alisema

Changamoto nje ya kundi?

Baada ya kutoka kwenye kundi mwanzoni mwa mwaka 2017 ,Aslay aliachia kibao chake cha Angekuona ambapo aliachia pamoja na video,Tarehe 10 mwezi wa nne na mpaka sasa imejikusanyia watazamaji milioni tatu na kuongeza kuwa changamoto kubwa anayokumbana nayo kwa sasa ni kujaribu kutaka kupendwa na kila mtu jambo ambalo ni kazi kutokea ila anajitahidi kuhakikisha mashabiki zake wengi wanaomkubali wazidi kufurahia kazi zake.

“Unajua ndani ya Bendi mko wengi kwahiyo chochote kikitokea wote kwa pamoja mnabeba msalaba lakini ukiwa peke yako kama hivi hasa unapojaribu kutaka kupendwa na watu hapo ndo changamoto huja sababu ni kazi sana unajua,” alisema

Nyimbo anazozikubali kutoka kwake?

“Napenda nyimbo zangu zote,lakini nazani nyimbo ambazo nazisikiliza sana ni Rudi pamoja na Angekuona nazipenda sana,”

Kuhusu Bendi Kufa

Aslay anasema kuwa suala la bendi mwenye majibu yote ni Mkubwa Fella na yeye hawezi kusema wazi kama bendi imekufa ama laah.
“Unajua suala la Ya Moto mwenye majibu yote ni Mkubwa Fella,lakini mimi kama baadae kuna mambo mengine yataendelea au kundi litahitaji tuendeleze kazi mimi nipo fresh ila majibu ya kufa kwa kundi mwenye majibu yote ni Mkubwa Fella,”

Mahusiano na Baba yake?

Hili halifichiki kuhusu suala la Aslay kuwa na mapenzi makubwa kwa Mama yake “Moza Mohamed”ambaye alifariki mwaka 2015 na hata wimbo Angekuona kwa asilimia kubwa unamuhusu Mama yake huyo.

Na pia kuna kipindi fulani iliwahi kudaiwa kuwa Aslay alikuwa akiishi na Mama yake tu huku Baba yake akiendelea kupambana na hali yake jambo lilionesha kama kuna kutokuelewana kati yake na Baba yake.

“Mimi na Mzee mbona fresh tunaonana tunapiga stori na mambo mengine,Mimi nawapenda Wazazi wangu japo Mama ametangulia mbele za haki lakini hata Baba tupo vizuri tunaongea mara kwa mara,”alisema

Jambo ambalo wengi hawajui kutoka kwa Aslay?

Anafunguka kuwa watu wengi kuna mambo kadhaa ambayo hawayajui na kusema hataki hata kidogo watu wayajue maisha yake binafsi.

“Kwanza watu hawajui mimi nina stoo ya nyimbo za kutosha sana,kiasi kwamba nikiamua kuachia kila siku wimbo mmoja mmoja sijui hata kwamba zitaisha lini,”

Mambo anayojutia

Anasema kuwa kwa upande wake hakuna kitu anachojutia katika maisha yake sababu anaona hakuna mtu yeyote aliyemkosea au kufanya jambo baya.

“Mimi naona niko fresh hakuna kitendo kibaya nimewahi kufanya au labda kuna mtu nilimkosea mimi naona niko fresh na wala sijutii lolote,”

Vipi kuhusu kolabo?

“Kwa sasa sifikirii kufanya kolabo lolote lakini sababu muziki nao kuna muda unaenda kwa upepo tunaweza kufikiria mbele,”

Mishe nyingine?

Aslay anasema kuwa hana mishe yoyote nyingine anayofanya zaidi ya Muziki na kwake anafunguka kuwa Muziki ndio kila kitu sababu ndio unaompa riziki yake ya kila siku na ndio maana anapambana kwa nguvu zote.

Kuhusu mpira yeye ni shabiki wa timu zipi?

Anafunguka kuwa yeye ni mpenzi mkubwa wa Simba,Chelsea pamoja na Real Madrid huku akiwataja wachezaji kama Samatta,Drogba pamoja na Mata kuwa ndio wanaomkosha zaidi.

Kama sio Muziki angekuwa anafanya nini?

“Kama isingekuwa Muziki basi ningekuwa nacheza mpira aisee maana ka kipaji kapo kapo,sidhani kama ningekuwa nasoma,”anasema

Shoo ambayo hawezi kusahau kwake?

“Ilikuwa Uingereza huko,Yamoto tulienda kupafomu huko aisee watu walijaa sana siku ile yani sikuamini nilihisi kama nipo Bongo kumbe nipo nje sitokuja kusahau siku ile,”

Anapenda msosi gani?
Wali Njegere

“Mimi napenda wali njegere aisee hapo haunitoi kabisa kabisa na mara nyingi naupiga sana huo mpaka najihisi hata njiani nitakuwa nanukia Wali njegere,”

Vipi kuhusu mahusiano yake?

Katika mahusiano yake Aslay amewahi kudaiwa kutoka na mwanamitindo na pia video queen akifahamika kwa jina la Tessy,Lakini mwanzo wa mwaka 2016 penzi lao liliota mbawa baada ya Tessy kushika mimba japo wote wawili walikana kwamba kuachana kwao Mimba haikua sababu.
Aslay na Tessy
Baadae tena,Aslay tetesi za chini ilidaiwa kuwa ana mahusiano na mwimbaji Ruby hasa baada ya kupostiana kwa sana katika Instagram zao na maneno kadhaa ambayo yalionesha kuna namna kati yao,japo wote walikana ishu hiyo.

Lakini kwa sasa ni kama mapenzi yake yamerudi kwa Mama mtoto wake ambapo nae Aslay alithibitisha hilo.

“Mimi sipendi kuongelea haya lakini kiufupi nina mtoto mmoja anaitwa Moza wengi wanajua,ni jina ambalo nilimpa kutokea kwa Mama yangu ambae ndio jina lake halisi na kwa sasa nipo na Tessy ambae ndio Mama pia wa mtoto wangu,”alisema.

Nini anapenda kufanya akiwa nyumbani?

“Mimi nikiwa nyumbani napenda sana kucheza PES(Gemu la mpira wa miguu) na timu ninayoipenda kuitumia ni Chelsea huwa nawapiga sana sema nao huwa wananiotea kimtindo,”
“Nimewahi kupigwa kumi aisee japo nilikuja kuzilipa kimbinde mbinde.”anaongeza

Mafanikio kutokea Youtube?

Katika video alizotoa katika mtandao wa Youtube zote zimeweza kufikisha watazamaji milioni moja ambapo Aslay anasema amepata faida kubwa sana katika hilo.

“Cha kwanza nimepata kipato na cha pili ni heshima sababu unajua kwanza kuna baadhi ya wasanii hawajawahi kufikisha watazamaji hao kwahiyo hivyo ni vitu viwili ninavyojivunia kupitia video zangu Youtube,”

Mipango ya baadae?

“Nina mipango mingi lakini kubwa namimi nataka nije kumiliki wasanii na hilo ndilo ninaliwaza sana kama mipango yangu itaenda poa natumaini hilo litawezekana,”

Historia fupi ya Aslay.

Kaka yake anaefahamika kwa jina la Idd ndiye aliyegundua kipaji chake baada ya kumuona mara kwa mara akipenda kuimba imba kila alipokaa. Alimchukua na kuamua kumpeleka kwa mdau mkubwa wa Muziki,Said Fella “Mkubwa” ambaye alipenda kipaji kutoka kwake na kuamua kumchukua na kuanza kumnoa ndani ya kituo cha vipaji cha Mkubwa na Wanawe.

Ndani ya kituo hicho Aslay alipigwa msasa wa nguvu na watu kama Yusuph Chambuso ambae kwa sasa ndiye meneja wake.

Mwaka 2011 alishiriki shoo ya Nchi za Majahazi maarufu kama (ZIFF) ambapo alipata nafasi ya kupafomu na kuimba wimbo wa “Zuwena” wimbo ambao ni wa marehemu Marijani Rajab “Jabali la Muziki”.

 Mwaka huohuo, 2011 akachomoka na ngoma yake ya kwanza,ambayo ilivuma kwa nchi nzima na kupendwa sana, iliyokwenda kwa jina la “Nakusemea”.

 Mwaka 2012 Aslay aliachia ngoma nyingine aliyoipa jina la “Umbea” ambayo alimshirikisha Chegge Chigunda.

Baada ya kuachia ngoma kadhaa tena kama Niwe Nawe na baadhi ya makolabo, ndipo mwishoni wa mwaka 2013, liliundwa kundi la Yamoto Bendi kwa kushirikisha pia vijana wengine watatu ambao ni Beka, Maromboso pamoja Enock Bella na hapo ndipo safari ilianza kwa moto mkali na mpaka sasa ambapo kila mmoja anapambana kivyake.

 






Pages