Rais wa Marekani Donald trump anaonekana kuwa ni kati ya Rais
ambao ni wakorofi na wasiopenda kuingiliwa katika mambo yao, lakini msanii
Webiro Noel Wasira ‘Wakazi’ yeye alikuwa miongoni mwa watu waliowahi kukutana
na Rais huyo wa sasa nchini Marekani.
Wakazi ni msanii wa miondoko ya Hip Hop ambaye alikuwa akiishi
nchini Marekani kwa muda mrefu, na kupata uzoefu wa nchi mbili tofauti kuanzia
katika maisha ya muziki mpaka maisha ya kawaida nje ya Muziki.
Mwananchi ilifanya naye mazungumzo kutaka kufahamu mengi juu
yake kutokana na kuwa ni miongoni mwa wasanii ambao waliweza kupafomu katika
jumba la Big Brother sehemu ambayo ni ngumu msanii wa kawaida kuipata.
ILIKUAJE KUTUA MAREKANI
“Nilienda kusoma Marekani lakini nilivyoenda kule nikajikuta
naendelea na Muziki kitu ambacho nilikuwa nakipenda tangu nikiwa nakaa
Tanzania, na watu wakubwa waliokuwa wakinifanya nipende Muziki ni watu mtaani
kwetu takishari kwasababu kwa miaka ya nyuma mtaa huu walikuwa wanakaa
mabalozi,”anasema.
“Hivyo nilivyoenda kusoma ikawa nafanya kitu ambacho nakipenda
kila siku lakini nashukuru Mungu nilikuwa nakifanya kwa umakini mkubwa,
nilihakikisha kuwa najulikana kule na hata nyumbani kwasababu unatakiwa uwe
unajulikana kuanzia nyumbani,”anasema.
ALIKUTANA VIPI NA TRUMP
“Nilivyokaa kwa miaka kadhaa maisha yalibadilika na ukiangalia
kuwa upo katika nchi ya watu, hivyo ikanibidi nianze kufanya kazi katika jengo
la Trump ‘Trump Tower’ na ndipo ambapo nilikutana na Trump na sio yeye pekee,
kwani jengo lile lilikuwa likitembelewa na watu wengi mno maarufu hivyo nikawa
nakutana na wasanii wakubwa pia,”anasema.
“Trump kwa kipindi chote ambacho nilikuwa nikifanya kazi ndani
ya jengo lake, nimeona ni mtu ambaye anajali watu na ni msikivu ila ukifanya
kitu ambacho hajakipenda ni mtu ambaye anachukua maamuzi ya haraka
mno,”anasema.
ALIWEZAJE KUJIPANGA KATIKA MASOMO,MUZIKI NA KAZI
“Ilikuwa ni wakati mgumu sana kwangu kwa namna moja ama
nyingine, kwasababu nilikuwa nchi ya watu na nilitakiwa niishi vizuri hivyo
licha ya kuwa nilikuwa ni mwanafunzi kule lakini ilibidi
nijichanganye,”anasema.
“Nilikuwa najipanga kuwa asubuhi kama nitaenda chuo basi
nikirudi napumzika, alafu naingia kazini katika upande wa muziki ilikuwa sio
shida sana, lakini inapotokea ishu ya kusafiri kwenda kufanya shoo ndio ilikuwa
changamoto kwasababu ilikuwa unatoka mji mmoja kwenda mji mwingine,kuna kipindi
niliacha mpaka Chuo”.
TOFAUTI YA HIP HOP YA BONGO NA MAREKANI
“Mziki haunaga tofauti yoyote, bali ni kuwa hapa nyumbani
haijatengenezwa fomula nzuri, kupigwa Muziki redioni haimaanishi kuwa umeuza,
Kuna watu wanakuwa na mixtape nyingi kule Marekani na wanapiga pesa kuliko
ambao wana nyimbo zao redioni, kitu ambacho ni tofauti na hapa
nyumbani,”anasema.
Pia aliongeza kuwa wasanii wengi wanakuwa na Identity
(Utambulisho) yao ya kutambulisha sehemu wanayotokea kama ambavyo alikuwa anafanya
50 Cent, Fat Joe kwa kutaja sehemu ambayo wanatokea na kisha watu wanaokaa
maeneo hayo kuanza kuwasapoti kwa kununua mixtapes (Kanda Mseto) zao.
ALIPATAJE NAFASI YA KUPIGA SHOW BBA
“Ile nafasi wengi hawakutarajia kama ningeipata, kutokana na
kuwa nyimbo zangu hazipigwi sana katika redio za nyumbani, lakini nilichokuwa
nakifanya mimi kwa miaka ile ni kuhakikisha kuwa naweka kazi mitandaoni ,
ukitafuta msanii ambaye anatoka Tanzania nilikuwa nipo katika orodha hiyo na
wakati ule Big brother walikuwa wanataka msanii ambaye anachipukia kutoka
Tanzania hivyo walivyotafuta waliniona mimi,”anasema.
ANAAMINI MITANDAO INALIPA
“Mitandao inalipa ndio kwasababu kama mtu akisikiliza wimbo
wako kupitia akaunti yako wewe pesa inaongezeka, utaitwa na kwenda kusaini na
kisha kuchukua pesa yako, na hicho ndicho kitu ambacho mimi nakifanya,”anasema.
Pia aliongeza kuwa kupitia mitandao inakuwa ni rahisi kufanya
wimbo na msanii kutoka nje kutokana na kufatilia kazi zako katika mtandao na kisha
kukutafuta, ni tofauti na kupigwa katika redio za nyumbani huku wasanii wa nje
hawasikii kazi zako.
BIFU LAKE NA GODZILA LIMEKAAJE
“Mimi na Zilla hatuna bifu la nje ya maisha ya kawaida, lakini
kilichotokea ni kuwa mimi nilitweet kwenye Twitter na yeye akaja kukomenti kitu
asichokijua na mimi nikamjibu hivyo watu wakaona yale mazungumzo yetu ghafla
yakawa makubwa mno”anasema.
“Nikapelekwa katika kituo kimoja cha Redio kwenda kumaliza
ubishi nay eye kwa kufanya mitindo huru na nilifanikiwa kufanya vizuri dhidi
yake, na baada ya hapo ikanibidi nitoe wimbo kuhusu yeye na yeye akatoa wimbo
kuhusu mimi yani ndio ikawa hivyo,”anaelezea.
NGUVU YA UMENEJA WA LADY JAYDEE
“Wengi hawajui kuwa mimi na Jide ni mtu na binamu yake, hivyo
kuwa meneja ilitokea tu baada ya kuwa aliyekuwa meneja wake kuacha kazi hiyo na
kutokana na ukaribu wangu na kujua ufanyaji wetu wa kazi ikabidi anikabidhi
jukumu hilo, lakini nashukuru nimelifanyia kazi vizuri eneo hilo,”anasema.
“Katika kipindi chote ambacho nimefanya kazi nimejifunza vitu
vingi, hakuwahi kunisumbua kwasababu ni mtu ambaye anajielewa sio msanii mpya,
na kuwa naye karibu kumenikutanisha na watu wengi na hata mimi pia nilikuwa
natumia nafasi hiyo kutangaza kazi zangu,”anasema.
KWANINI SHOO ZA HIP HOP ZINAKUWA NA VIINGILIO VIDOGO
“Uzuri ni kwamba nimeshakuwa meneja wa Jaydee kwahiyo najua
kabisa kuwa upande wa pili wa shilingi wanafaulu vipi, kikubwa ukiwa unataka
kuweka kiingilio kikubwa unatakiwa uonyeshe jinsi ambavyo ela yao
inavyotumika”, anasema.
Aliongeza kuwa huwezi kuweka kiingilio kikubwa na ukawa hauna
vitu vingi kama live band, hivyo ni muhimu kuhakikisha kuwa unakuwa na vitu
vingi ambavyo hata mtu anayetoa pesa yake anapata kitu kinachoendana, ila kwa
upande wetu sisi kiukweli bado inabidi nguvu iongezeke zaidi japokuwa katika matamasha
makubwa,huwa tunafanya vitu vikubwa hasa kwa kutumia sauti halisi bila Cd.
AWAKATAA KIAINA MADIREKTA WAKUBWA
“Naweza kusema kuwa nilikuwa na mtayarishaji mkubwa Hefemi
ambaye ni Mtanzania anayeishi Marekani, yeye ndio alikuwa anatayarisha kazi zangu
nyingi nilipokuwa nje ya nchi lakini hata niliporudi alikuwa anatayarisha na
kazi zilikuwa zinafanya vizuri,”
“Uzuri wa kazi sio mtayarishaji mkubwa kwani baada ya Hefemi
nilihamia kwa Meck Kaloka ambaye nilimsihi aongozane na Hefemi ili ajue aina ya
video zinazohitajika na ndio maana mpaka hivi sasa video zangu zinafanya
vizuri, na kupitia Meck Kaloka nyimbo ya ‘Dengue Fever’ ambayo niliifanya
kwa gharama ya chini lakini ilinifanya niingie katika tuzo za Kora,Tuzo ambazo
ni kubwa mno kwa hapa Africa,”anasema.
ANAMZUNGUMZIAJE HASHEEM THABEET
“Alikuwa ni mtu mzuri kwangu kwasababu tulikuwa tunaishi
vizuri tulipokuwa wote Marekani, na ilifika kipindi hata natakiwa niende katika
mji mwingine alikuwa akinisaidia hata mafuta ya kunisogeza, na hali hiyo iliendelea
mpaka alipoingia NBA ni mtu mzuri sana na niliishi nae vizuri,”
“Najua kuwa hivi sasa anajifua na mazoezi binafsi ili aweze
kurudi katika NBA, ila ni ngumu sana na yeye analijua na Watanzania wanaoishi
kule wanalijua kwasababu kupata nafasi NBA ni mpaka mtu aumie au kiwango chake
kishuke, hivyo ataangalia kama hatopata pale nafasi anaweza akatafuta sehemu
nyingine,”anasema.
UPANDE WA SIASA YUPOJE
Wakazi licha ya kuwa anamuita Baba Mdogo Steven Wasira, yeye
amefunguka kuwa hajihusishi na Siasa kutokana na siasa kuwa na mambo mengi, pia
siasa inakuwa aina marafiki wa kweli ambao wanaweza kumsaidia mtu katika
kipindi anachohitaji.
“Mimi Siasa ya Jamii, Uraia sijihusishi nayo kabisa,
najihusisha na siasa ya nchi kwasababu mimi ni mfanyabiashara na biashara yangu
ni muziki, na mziki ninaofanya ni siasa pia kwasababu ni mziki wa kweli na upo
wazi, katika upande wa kupiga kura huwa naangalia utendaji wake wa kazi na ndio
napiga kula lakini huwa siangalii chama,”
WASANII ANAOWAKUBALI KUPITIA IDADI ZAO ZA KAZI
Wakazi alisema kuwa wasanii anaowakubali ni watano na ni
kutokana na idadi zao za kazi ambazo wamezifanya mpaka hivi sasa, huku wakiwa
wanaendelea na muziki kama kawaida hivyo ni ngumu kufikiwa.
MWISHO
No comments:
Post a Comment