Ilinichukua masaa matano kuweza kukutana na Aslay,huku masaa
manne yakipotea kwa kumsubiri na moja likitumika kwa kazi maalumu ambayo ndiyo
ilinifanya nimtafute na kumsubiri, na si kingine bali ni mahojiano.
Kwa sasa jina la Aslay kwa Bongo,lipo katika levo za juu na
hii inawezekana ikawa ndiyo sababu ambayo kuweza kupata nafasi ya kufanya nae
mahojiano yakupasa uwe mvumilivu sana sababu ya ubize mkali kutokana na
kuzunguka mikoa mbalimbali kupiga shoo huku akifanya mambo mengine mbalimbali
ambayo hapendi kuyaweka wazi.
“Aisee pole sana ndugu yangu kwa kukuweka sana,” Alianza Aslay
mara baada ya kuonana nae huku nae akionekana kuchoka ambapo alianza kwa
kulalamika njaa .
Mahojiano yalianza mara moja sababu kwa saa lingine ambalo
lilikuwa linafuata alikuwa anatakiwa eneo lingine hivyo haikutakiwa kulaza
damu.
Kwanini
Nyimbo Mfululizo?
Moja ya kitu ambacho wengi wamekuwa wakitaka kujua ni kwanini
anaachia ngoma mfululizo,ambapo mpaka sasa ameachia video saba huku kila video
ikipishana kwa mwezi mmoja mmoja,kwa maana kwamba kila baada ya mwezi kupita
amekuwa akiachia video.Video hizo ni kama Angekuona,Baby,Usiitie Doa aliyofanya
na Khadija Kopa,Muhudumu,Pusha,Likizona Natamba Na kwa upande wa Audio mpaka sasa
kupitia akaunti yake ya Youtube zipo kumi na mbili tu ambazo ni Pusha,Usiitie
Doa,Baby,Danga,Koko,Rudi,Hutegeki,Muhudumu,Likizo,Marioo,Natamba na Tete,lakini
zinazidi idadi hiyo kwa sababu kuna nyimbo nyingine ambazo zipo mitaani kama
Nyakunyaku pamoja na singo kadhaa.
Akijibu hilo Aslay anasema kwake anafanya hivyo kwa sababu
anaamini muziki mzuri hauwezi kufa hata kidogo.
“Kwanza Muziki mzuri haufi hata siku moja lazima watu wajue,na
kingine mimi nimeamua kuachia nyimbo mfululizo sababu nilitaka kuwa na nyimbo
za kutosha hata nikienda kufanya shoo mashabiki zangu waweze kufurahi nyimbo
zangu na sio tena za Ya Moto Bendi,”
“Na pia nilipoteza flash yenye nyimbo lakini ilikuwa muda sana
japo niliogopa kwamba nyimbo zangu zisije kuanza kuvuja lakini namshukuru Mungu
haikuwa hivyo ila sababu kubwa ndio hiyo niliyosema,”
“Na kuhusu kuendelea ama kuacha kuachia ngoma kama hivi hiyo
ndio fomula yangu ila nitakuwa naangalia upepo unaendaje sababu wasinione
mjinga pia,”
Meneja
wake kwa sasa?
Baada ya kuachana na Mkubwa Fella,Aslay anasema kwa sasa kazi
zake anasimamiwa na Chambuso hivyo kwa watu ambao walikuwa wakifikiri kwamba
hana msimamizi yeyote ndio waanze kujua hilo.
“Huyu ndio meneja wangu kila kitu kuhusu muziki wangu na mambo
mengine mbalimbali yeye ndiye anasimamia, nashukuru anafanya kile ambacho
nakipenda haswa,”
Kuhusu
Nyumba?
Katika suala la Nyumba ambazo inadaiwa walikuwa wakijengewa
kipindi wapo Yamoto na kuna tetesi zilikuwa zikiendelea kuwa Nyumba hizo
ziliota mbawa,Aslay anajibu kuwa nyumba hizo zipo na si kweli kama wengi
walivyokuwa wanasema.
“Nyumba zipo tulijengewa wote Mbagala eneo moja na mpaka sasa
naweza kusema zina hadhi kweli ya mtu kuishi,”alisema
Changamoto
nje ya kundi?
Baada ya kutoka kwenye kundi mwanzoni mwa mwaka 2017 ,Aslay aliachia
kibao chake cha Angekuona ambapo aliachia pamoja na video,Tarehe 10 mwezi wa
nne na mpaka sasa imejikusanyia watazamaji milioni tatu na kuongeza kuwa changamoto
kubwa anayokumbana nayo kwa sasa ni kujaribu kutaka kupendwa na kila mtu jambo
ambalo ni kazi kutokea ila anajitahidi kuhakikisha mashabiki zake wengi
wanaomkubali wazidi kufurahia kazi zake.
“Unajua ndani ya Bendi mko wengi kwahiyo chochote kikitokea
wote kwa pamoja mnabeba msalaba lakini ukiwa peke yako kama hivi hasa
unapojaribu kutaka kupendwa na watu hapo ndo changamoto huja sababu ni kazi
sana unajua,” alisema
Nyimbo
anazozikubali kutoka kwake?
“Napenda nyimbo zangu zote,lakini nazani nyimbo ambazo
nazisikiliza sana ni Rudi pamoja na Angekuona nazipenda sana,”
Kuhusu
Bendi Kufa
Aslay anasema kuwa suala la bendi mwenye majibu yote ni Mkubwa
Fella na yeye hawezi kusema wazi kama bendi imekufa ama laah.
“Unajua suala la Ya Moto mwenye majibu yote ni Mkubwa
Fella,lakini mimi kama baadae kuna mambo mengine yataendelea au kundi litahitaji
tuendeleze kazi mimi nipo fresh ila majibu ya kufa kwa kundi mwenye majibu yote
ni Mkubwa Fella,”
Mahusiano
na Baba yake?
Hili halifichiki kuhusu suala la Aslay kuwa na mapenzi makubwa
kwa Mama yake “Moza Mohamed”ambaye alifariki mwaka 2015 na hata wimbo Angekuona
kwa asilimia kubwa unamuhusu Mama yake huyo.
Na pia kuna kipindi fulani iliwahi kudaiwa kuwa Aslay alikuwa
akiishi na Mama yake tu huku Baba yake akiendelea kupambana na hali yake jambo
lilionesha kama kuna kutokuelewana kati yake na Baba yake.
“Mimi na Mzee mbona fresh tunaonana tunapiga stori na mambo
mengine,Mimi nawapenda Wazazi wangu japo Mama ametangulia mbele za haki lakini
hata Baba tupo vizuri tunaongea mara kwa mara,”alisema
Jambo
ambalo wengi hawajui kutoka kwa Aslay?
Anafunguka kuwa watu wengi kuna mambo kadhaa ambayo hawayajui
na kusema hataki hata kidogo watu wayajue maisha yake binafsi.
“Kwanza watu hawajui mimi nina stoo ya nyimbo za kutosha
sana,kiasi kwamba nikiamua kuachia kila siku wimbo mmoja mmoja sijui hata kwamba
zitaisha lini,”
Mambo
anayojutia
Anasema kuwa kwa upande wake hakuna kitu anachojutia katika
maisha yake sababu anaona hakuna mtu yeyote aliyemkosea au kufanya jambo baya.
“Mimi naona niko fresh hakuna kitendo kibaya nimewahi kufanya
au labda kuna mtu nilimkosea mimi naona niko fresh na wala sijutii lolote,”
Vipi
kuhusu kolabo?
“Kwa sasa sifikirii kufanya kolabo lolote lakini sababu muziki
nao kuna muda unaenda kwa upepo tunaweza kufikiria mbele,”
Mishe
nyingine?
Aslay anasema kuwa hana mishe yoyote nyingine anayofanya zaidi
ya Muziki na kwake anafunguka kuwa Muziki ndio kila kitu sababu ndio unaompa
riziki yake ya kila siku na ndio maana anapambana kwa nguvu zote.
Anafunguka kuwa yeye ni mpenzi mkubwa wa Simba,Chelsea pamoja
na Real Madrid huku akiwataja wachezaji kama Samatta,Drogba pamoja na Mata kuwa
ndio wanaomkosha zaidi.
Kama sio
Muziki angekuwa anafanya nini?
“Kama isingekuwa Muziki basi ningekuwa nacheza mpira aisee
maana ka kipaji kapo kapo,sidhani kama ningekuwa nasoma,”anasema
Shoo
ambayo hawezi kusahau kwake?
“Ilikuwa Uingereza huko,Yamoto tulienda kupafomu huko aisee
watu walijaa sana siku ile yani sikuamini nilihisi kama nipo Bongo kumbe nipo
nje sitokuja kusahau siku ile,”
“Mimi napenda wali njegere aisee hapo haunitoi kabisa kabisa
na mara nyingi naupiga sana huo mpaka najihisi hata njiani nitakuwa nanukia
Wali njegere,”
Vipi
kuhusu mahusiano yake?
Katika mahusiano yake Aslay amewahi kudaiwa kutoka na
mwanamitindo na pia video queen akifahamika kwa jina la Tessy,Lakini mwanzo wa
mwaka 2016 penzi lao liliota mbawa baada ya Tessy kushika mimba japo wote
wawili walikana kwamba kuachana kwao Mimba haikua sababu.
Aslay na Tessy |
Baadae tena,Aslay tetesi za chini ilidaiwa kuwa ana mahusiano
na mwimbaji Ruby hasa baada ya kupostiana kwa sana katika Instagram zao na
maneno kadhaa ambayo yalionesha kuna namna kati yao,japo wote walikana ishu
hiyo.
Lakini kwa sasa ni kama mapenzi yake yamerudi kwa Mama mtoto
wake ambapo nae Aslay alithibitisha hilo.
“Mimi sipendi kuongelea haya lakini kiufupi nina mtoto mmoja
anaitwa Moza wengi wanajua,ni jina ambalo nilimpa kutokea kwa Mama yangu ambae
ndio jina lake halisi na kwa sasa nipo na Tessy ambae ndio Mama pia wa mtoto
wangu,”alisema.
“Mimi nikiwa nyumbani napenda sana kucheza PES(Gemu la mpira
wa miguu) na timu ninayoipenda kuitumia ni Chelsea huwa nawapiga sana sema nao
huwa wananiotea kimtindo,”
“Nimewahi kupigwa kumi aisee japo nilikuja kuzilipa kimbinde
mbinde.”anaongeza
Mafanikio
kutokea Youtube?
Katika video alizotoa katika mtandao wa Youtube zote zimeweza
kufikisha watazamaji milioni moja ambapo Aslay anasema amepata faida kubwa sana
katika hilo.
“Cha kwanza nimepata kipato na cha pili ni heshima sababu
unajua kwanza kuna baadhi ya wasanii hawajawahi kufikisha watazamaji hao
kwahiyo hivyo ni vitu viwili ninavyojivunia kupitia video zangu Youtube,”
Mipango
ya baadae?
“Nina mipango mingi lakini kubwa namimi nataka nije kumiliki wasanii
na hilo ndilo ninaliwaza sana kama mipango yangu itaenda poa natumaini hilo
litawezekana,”
Kaka yake anaefahamika kwa jina
la Idd ndiye aliyegundua kipaji chake baada ya kumuona mara kwa mara akipenda
kuimba imba kila alipokaa. Alimchukua na kuamua kumpeleka kwa mdau mkubwa wa
Muziki,Said Fella “Mkubwa” ambaye alipenda kipaji kutoka kwake na kuamua
kumchukua na kuanza kumnoa ndani ya kituo cha vipaji cha Mkubwa na Wanawe.
Ndani ya kituo hicho Aslay
alipigwa msasa wa nguvu na watu kama Yusuph Chambuso ambae kwa sasa ndiye
meneja wake.
Mwaka 2011 alishiriki shoo ya
Nchi za Majahazi maarufu kama (ZIFF) ambapo alipata nafasi ya kupafomu na
kuimba wimbo wa “Zuwena” wimbo ambao ni wa marehemu Marijani Rajab “Jabali la
Muziki”.
Mwaka huohuo, 2011 akachomoka na ngoma yake ya
kwanza,ambayo ilivuma kwa nchi nzima na kupendwa sana, iliyokwenda kwa jina la
“Nakusemea”.
Mwaka 2012 Aslay aliachia ngoma nyingine
aliyoipa jina la “Umbea” ambayo alimshirikisha Chegge Chigunda.
Baada ya kuachia ngoma kadhaa
tena kama Niwe Nawe na baadhi ya makolabo, ndipo mwishoni wa mwaka 2013,
liliundwa kundi la Yamoto Bendi kwa kushirikisha pia vijana wengine watatu
ambao ni Beka, Maromboso pamoja Enock Bella na hapo ndipo safari ilianza kwa
moto mkali na mpaka sasa ambapo kila mmoja anapambana kivyake.