Ufanye Nini Unapofanya Maamuzi Ya Kununua Laptop?#Uchambuzi - teknomovies
Ufanye Nini Unapofanya Maamuzi Ya Kununua Laptop?#Uchambuzi

Ufanye Nini Unapofanya Maamuzi Ya Kununua Laptop?#Uchambuzi

Share This

Pale unapofanya maamuzi ya kununua laptop ni muhimu sana ufanye maamuzi mazuri kwani ni mara chache sana watu huwa wanabadilisha laptop haraka haraka.

Leo tutakusaidia jinsi ya kuhakikisha unapata kitu kizuri pale unapofanya maamuzi ya kununua laptop.

> Laptop ya Windows, Ubuntu (Linux) au Macbook (Apple)?

Point hii ni muhimu kwa sababu mbalimbali. Kompyuta/Laptop za MacBook ni ghari zaidi ukilinganisha na laptop inayotumia Windows tena ata zile zenye uwezo mkubwa zaidi kuliko ata hiyo ya MacBook.

Kingine ni kwamba kama unaujuzi wa kuinstall programu endeshaji ya Windows mwenyewe basi unaweza jikuta ukaokoa kati ya TSh 150,000 hadi Tsh 250,000 ukinunua laptop inayokuja na programu endeshaji ya Linux (Ubuntu n.k) au ata zile ambazo hazijaweka programu endeshaji yeyote (DOS) ukilinganisha na kama ukinunua laptop hiyo hiyo huku ikiwa tayari imewekwa Windows 7 – 10.


> Diski Uhifadhi ya teknolojia ya SSD, HDD au Hybrid (SSD+HDD)?

Teknolojia ya diski uhifadhi ya SSD ni ya kisasa zaidi na inahakikisha kompyuta yako inafanya kazi kwa ufanisi zaidi. Ila ubaya ni mmoja tuu, mara nyingi kwenye laptop diski za SSD zinakuwa ni za ujazo mdogo na pia bei inakuwa juu kidogo.

Kama pesa ipo vizuri basi ni bora upate laptop inayokuja na diski C ya SSD na diski D ya HDD (yaani Hybrid). Hii itahakikisha unanufaika na ufanisi mzuri zaidi wa programu endeshaji wakati huo huo unapata nafasi kubwa ya ujazo kupitia HDD.

> Je huwa una matumizi ya aina gani?

Hili ni jambo la muhimu sana kufahamu kabla ya kwenda dukani kununua laptop ambayo baada ya muda ndio ukaona ya kwamba hukuchagua laptop ambayo ilikuwa sahihi kwa kazi zako.

Kama mara nyingi kazi zako zinakufanya uwe mbali na maeneo ya kuchaji basi hakikisha unanunua laptop yenye kiwango kikubwa zaidi cha kukaa na chaji. Siri moja wapo ni kwamba chagua laptop zenye prosesa za kisasa zaidi (5th Generation) hizi zinatumia chaji kidogo zaidi ukilinganisha na laptop zenye prosesa za zamani.


Kama pia unanunua kwa ajili ya matumizi pia ya kutazama filamu n.k basi ukubwa wa kioo chake (Screen) itakuwa ni muhimu pia.


Je wewe ni mtu wa mishe mishe mingi? Basi laptop kubwa sana itakuletea mzigo sana katika suala la ubebaji, basi chagua zile ambazo ni nyepesi.


Je utaitumia ata muda usiku na eneo lenye mwanga mdogo au chumbani nyakati za usiku? Basi hakikisha unachagua laptop yenye kutoa mwanga hadi eneo la keyboard. Hii itakusaidia uwezo wa kuchapa vizuri bila wasiwasi ata gizani.

> Unaitaji kweli eneo la DVD?

Ingawa bado laptop zenye eneo la DVD zinapatikana bali siku hizi ni kawaida kabisa kwa mtumiaji wa laptop kutopata kazi yake yeyote itakayoitaji utumiaji wa eneo la CD/DVD mwaka mzima. Kila kitu kinaweza fanyika kwa kutumia diski za USB.

Laptop zisizo na eneo la DVD mara nyingi zinakuwa nyepesi na nyembamba zaidi.

> Una mpango wa kuitumia kwa muda mrefu zaidi?

Kama jibu ni ndiyo basi hakikisha una chagua laptop yenye RAM nyingi zaidi kulingana na bajeti yako, tunashauri GB 8 – 16. Pia na prosesa ya kisasa. Hii ni kwa sababu suala hili litaipa kompyuta yako uhakika wa kuendelea kuwa na uwezo wa kupakua na kutumia app/programu nyingi za kisasa katika miaka 4 – 7 baadae.

Pia hakikisha unachagua laptop yenye jumba lenye kuduma misukosuko (case/body). Chagua zenye jumba la alumini/bati badala ya la plastiki isiyo kuwa bora.


Kingine muhimu ni kwamba hakikisha unalinganisha bei ya laptop uitakayo kutoka vyanzo vingine mbalimbali, ni kawaida kukuta laptop ile ile inauzwa kwa bei pungufu sehemu nyingine.
Haya ni machache muhimu ya kuzingatia. Je wewe una tazama mambo gani hasa? Tungependa kusikia.

chanzo:Mtandao wa Teknolojia wa Teknokona

Pages