JONAS SALK MGUNDUZI WA CHANJO YA POLIO,UGONJWA ULIOUA WATU WENGI SANA - teknomovies
JONAS SALK MGUNDUZI WA CHANJO YA POLIO,UGONJWA ULIOUA WATU WENGI SANA

JONAS SALK MGUNDUZI WA CHANJO YA POLIO,UGONJWA ULIOUA WATU WENGI SANA

Share This
Jonas Edward Salk alikuwa mwana Sayansi na mtafiti wa KiMarekani aliyegundua chanjo ya dhidi ya Ugonjwa wa Polio.

Jonas alizaliwa tarehe 28, mwezi Oktoba, mwaka 1914. Alizaliwa katika mji wa New York nchini Marekani kwa wazazi wenye asili ya Kiyahudi.

Pamoja na kwamba wazazi wake hawakuwa na elimu ya kutosha, walitamani sana kuona watoto wao wanapata Elimu bora.

Akiwa na miaka kumi na tatu (13) tu aliingia “Townsend Harris High School”, shule iliyokuwa imetengwa maalumu kwa ajili ya watu wenye vipaji

Baada ya kumaliza, alijiunga na chuo cha “City College of New York” ambapo alichukua “Bachelor of Science ”, na hatimaye kujiunga na “New York University School Of Medicine” aliposomea Udaktari.

Baada ya kumaliza shule, Jonas Salk aliamua kujishughulisha zaidi na shughuli za Utafiti, kuliko Udaktari wa wodini.

POLIO:

Ugonjwa wa Polio, ni ugonjwa wa kuambukiza unaosababishwa na “Polio Virus”.
Ugonjwa huu unaathiri misuli na mfumo wa Fahamu, hivyo kusababisha kupooza kwa viungo hasa miguu, na hata kifo.

Ulemavu huu ukishajitokeza huwa ni wa kudumu.
Waathirika wakuu wa Ugonjwa huu ni watoto, hasa walio na umri chini ya miaka mitano…
Kabla ya mwaka 1957, ambapo Jonas Salk aligundua chanjo ya Polio; Ugonjwa huo ulikuwa tishio kubwa sana nchini Marekani.

Kwa mfano: Mwaka 1952, zaidi ya kesi 58,000 za wagonjwa wa Polio ziligundulika nchini humo, na katika hao; takribani watu 3,145 walipoteza maisha, na wengine 21,269 kuachwa wamepooza.
Cha kusikitisha zaidi: asilimia kubwa ya waathirika walikuwa ni watoto.

Kutokana na hali hiyo hiyo, wanasayansi na watafiti wengi, walikuwa wakijaribu kwa kila namna kuweza kupata tiba ya ugonjwa huo. Raisi wa Marekani kipindi hicho; Bwana Franklin D. Roosevelt alizindua
organization iliyoitwa “March of Dimes Foundation” kwa ajili ya kusaidia na kufadhili utafiti wa kuutokomeza Ugonjwa huo.

Mwaka 1947, Jonas Salk aliteuliwa na chuo cha “University of Pittsburgh School of Medicine ” ili kuweza kusimamia project iliyofadhiliwa na “National Foundation for Infantile Paralysis” iliyokuwa na lengo la kuweza kutathmini aina mbalimbali za virusi vya polio.

Salk, aliiona hii kama fursa ya kuweza kutafuta chanjo dhidi ya polio.
Yeye, pamoja na timu ya watafiti aliowachagua, walianza kufanya tafiti zilizowachukua hadi miaka saba (7) ili kuweza kupata chanjo dhidi ya Ugonjwa huo.

Hatimaye tarehe 12, Aprili, 1955 ilitangazwa kwenye vyombo vya Habari, kwamba Salk na timu yake walikuwa wamefanikiwa kupata chanjo dhidi ya Ugonjwa huo mbaya.
Alisherekewa nchini humo kama mmoja ya mashujaa wakubwa, na kidogo siku hiyo iwe sikukuu ya Taifa.

Kupitia chanjo hiyo, mamilioni ya watu na haswa watoto, ikiwemo mimi na wewe tumeweza kuuepuka ugonjwa huu, kwa chanjo za polio tulizopata tulipozaliwa… na hii yote ni kwa ajili ya jitihada za Jonas Salk, pamoja na timu yake ya watafiti.

Kitu nilichokipenda zaidi kwa Salk, ni kwamba: baada ya Chanjo hiyo kupatikana, angeweza kuiwekea hatimiliki, na kutajirika kwa mauzo yake, kama ambavyo makampuni mengi ya madawa yanafanya hivi sasa… Lakini, alipoulizwa kama angeiwekea hatimiliki chanjo hiyo, alijibu: “Siwezi kuiwekea hatimiliki, Je Waweza kuliwekea hatimiliki Jua? ”

Jonas Salk, aliendelea na shughuli zake za Utafiti. Mwaka 1960, alizindua kitengo chake cha “Salk Institute for Biological Studies” kilichopo California mpaka leo kikiendelea kufanya tafiti mbalimbali.

Jonas Salk alitumia siku za mwisho za maisha yake akifanya tafiti ili kupata chanjo dhidi ya UKIMWI… Hatimaye alifariki tarehe 23, Juni, 1995.

Jonas Salk pia, ni moja kati ya mashujaa wangu (one of my heroes).

No comments:

Post a Comment

Pages